Abdilatif Abdalla alihojiwa kwa simu na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani, Mohamed Dahman. Mahojiano haya yalitangazwa katika kipindi, Dunia Yetu, baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa Kenya mwaka 2002, na siku moja baada ya Mwai Kibaki kuapishwa kuwa Rais mpya wa Kenya.
UTANGULIZI (MOHAMED DAHMAN): Mnasikiliza “Dunia Yetu” leo asubuhi kutoka Radio Deutsche Welle, Cologne. Na sasa umewadia wakati wa kuwadondolea yale yaliyoko katika safu yetu ya uchunguzi kutoka hapa na pale ulimwenguni. Asubuhi ya leo, mwanaharakati mashuhuri wa Kenya, Abdilatif Abdalla, anajiunga nasi kuzungumzia matarajio ya Wakenya kufuatia ushindi mkubwa wa kihistoria, wa muungano wa upinzani wa NARC, uliokiondoa chama cha KANU madarakani.
Kenya imepata Rais mpya, Mwai Kibaki, ambaye jana ameapishwa kushika wadhifa huo, kufuatia ushindi mkubwa wa muungano wa upinzani wa NARC dhidi ya chama cha KANU kilichokuwa kikitawala nchini humo, ambacho kilikuwa madarakani tokea uhuru wa nchi hiyo hapo mwaka 1963.
Abdilatif Abdalla ni mwanaharakati wa mageuzi ya Kenya tokea miaka ya 1960. Hapo mwaka 1966 alijiunga na chama cha upinzani cha KPU cha Jaramogi Oginga Odinga, na kuja hata kutumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani, kuanzia mwaka 1968, chini ya utawala wa rais wa kwanza wa Kenya huru, Jomo Kenyatta, kwa kuandika makala zenye kukosoa serikali. Baadaye aliendeleza harakati hizo kupitia chama cha MWAKENYA, kilichokuwa kikiendesha harakati zake chini kwa chini katika miaka ya 1980. Asubuhi hii, Abdilatif Abdalla, ambaye hivi sasa ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Leipzig hapa Ujerumani, amepata fursa ya kujiunga nasi. Na kwanza kabisa anatuelezea jinsi alivyozipokea habari hizo za Wakenya kuleta mabadiliko nchini mwao kwa njia ya kidemokrasia.
ABDILATIF: Imani yangu ni kwamba Wakenya hawataona kwamba hii ni hatua ya mwisho wakaanza kulala, bali hii ni hatua mojawapo tu ya kwendea kwenye lengo ambalo Wakenya wengi wanalitaka. Lakini kwa jumla ni habari ya furaha.
Halafu kumewekewa matarajio makubwa sana kwa Kibaki na muungano wake huu wa upinzani wa NARC: kwamba ameahidi kuwa Kenya sasa itakuwa na elimu bure ya msingi, ameahidi pia kwamba ataondoa utawala wa rushwa kwa sababu Kenya imeorodheshwa kuwa ni nchi mojawapo yenye serikali iliyotopea rushwa duniani. Halafu pia kuna swala la kufufua uchumi wa nchi uliozorota mno; miundombinu ya Kenya pia iko katika hali mbaya; serikali imeambiwa kwamba siyo safi, haifanyi kazi. Kwa hiyo sasa watu wanataka serikali safi inayowajibika, inayoaminika. Kwa hiyo ukitizama, Abdilatif, mambo hayo ni mengi, makubwa, na utekelezaji wake utahitaji wakati. Huoni hapa kwamba panaweza pakazuka kishindo?
Abdilatif: Kwa upande mmoja inaeleweka - kwamba kwa sababu nchi ya Kenya imekuwa katika hali hiyo mbaya kwa muda mrefu sana, kwa hivyo itakuwa ni kazi kubwa. Hizo ahadi zilizotolewa ni ahadi ambazo, kwa hakika, maadamu kuna nia – na iwe ni nia swafi na nia thabiti – nafikiri Wakenya kwa kuwa wamechoka na hali hii (na hapa haitategemea serikali peke yake, maana serikali peke yake haiwezi kufanya kitu, wala viongozi hao watakaounda serikali, peke yao hawataweza kutimiza lolote, ikiwa Wakenya wenyewe nao hawatashiriki na kushirikishwa katika kuibadilisha hali hii). Kwa hivyo, ikiwa kutakuwa na siasa nzuri na nia - tena thabiti na swafi - nina hakika mambo yataweza kutengenea, lakini yatachukua muda mrefu. Na Wakenya yataka wasiwe na pupa na haraka ya kutaka mambo yabadilike haraka haraka, maana hayataweza kubadilika.
Na tukija kwa upande wa KANU na Moi, wengi wanasema kwamba kitu ambacho watu hawawezi kukanusha kwamba ni mchango mkubwa wa Moi kwa Kenya – au tuseme, labda, ni hazina ya maana aliyowaachia Wakenya - ni amani: kwamba wakati wa utawala wake amejitahidi sana kuhakikisha kwamba amani inadumu Kenya.
Abdilatif: Katika hizi harakati za kisiasa, kuna watu chungu nzima ambao kwa muda wote huu ambao KANU imekuwa katika utawala, wameuwawa; watu wengine wamefungwa magerezani; watu wengine wameteswa kwa sababu ya kuwa na ujasiri wa kusema tu kwamba mambo yanakwenda vibaya na ni lazima yabadilike; na mambo mengine kadha wa kadha. Kwa hivyo, ikiwa watu wenyewe (walikuwa) hawana usalama, watu wenyewe (walikuwa) hawana hakika mtu kesho akiamka atakula nini, au mtoto wake akiwa mgonjwa (alikuwa) hana pesa za kumpelekea hospitali; hiyo pia ni sehemu katika amani ya nchi (ambayo haikuwako).
Halafu imeelezwa pia kwamba huu ushindi wa NARC umetokana na vitu viwili: kura ya kuukataa utawala (yaani kuikataa KANU na Moi), na matokeo – wanachosema kwamba – kama vile ni ya mapinduzi yaliyokuwa yakitokota kwa miezi sita iliyopita. Tukija kwa upande huo wa mapinduzi, changamoto kubwa mara nyingi inaonekana baada ya mapinduzi. Kwani ni kawaida kwa mapinduzi kuwala watoto wake wenyewe. Je, kwa upande wa NARC jambo hili halitotokea na kuja kusambaratisha chama hicho?
Abdilatif: Naam, kama ilivyo kawaida tena, wanasiasa wengi wamejiunga na NARC zaidi kwa maslahi yao ya binafsi kuliko kwa maslahi ya nchi au kwa maslahi ya wananchi wa Kenya. Kwa hivi sasa itaonekana kwamba labda wote wameshikamana. Lakini baada ya muda fulani kupita (na ikiwa serikali mpya hii kweli inataka kuleta mabadiliko, sioni vipi katika baadhi ya viongozi ambao wamo katika NARC hivi leo wataweza kuwa na madaraka katika serikali hii ya sasa). Maanake ni watu wale wale ambao walikuwa katika serikali ya KANU iliyopita, na wamefanya vitendo vichafu kabisa vya kuihujumu nchi na kuwahujumu wananchi, kwamba watu hawa wataweza kubadilika. Mimi hilo nina wasiwasi nalo sana. Kwa hivyo, hii ni hatua ya kwanza tu. Nina hakika kila tukiendelea mbele huko, ni lazima itabidi kuweko na mchujo mkubwa sana ikiwa kunatakikana kupatikane mabadiliko ya kweli katika nchi ya Kenya.
Abdilatif Abdalla, mwanaharakati mashuhuri wa mageuzi nchini Kenya.
- MWISHO -




